Na Mwandishi Wetu

LICHA ya Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuzuia uuzaji wa petroli kwenye vidumu, bado wamiliki wa vituo vya mafuta kwenye maeneo mbalimbali nchini wanaendelea na mtindo huo.

Lengo la Serikali kuzuia uuzaji huo wa mafuta, ni kudhibiti matukio ya mali za watu kuchomwa moto zikiwemo nyumba na magari na hilo ni kutokana na urahisi wa upatikanaji wa nishati hiyo.

Hata hivyo, imebainika maeneo mengi bado wamiliki wa vituo vya mafuta wamekahidi agizo hilo ambalo limekuwa likirudiwa mara kadhaa na mamlaka husika, ambapo moja ya vituo vinavyotajwa zaidi kufanya biashara hiyo ni JBS, kilichopo Bariadi, Mkoani Simiyu.

Kituo hicho ambacho kinatajwa kumilikiwa na mfanyabiashara John Sabu, ambaye ni baba mzazi wa Lucy Sabu, mbunge wa Viti Maalum kupitia Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM), kinadaiwa kuendesha biashara hiyo kwa muda mrefu.

“Serikali yetu inapaswa kuwa makini sana na kufuatilia hawa wamiliki wa vituo vya mafuta, wanakiuka taratibu nyingi za uendeshaji wa vituo hivi, kwa mfano hapa kwetu Bariadi, kituo hiki cha JBS biashara kubwa wanayoifanya ni kuuza mafuta kwenye vidumu na chupa za maji,”

“Ni wazi kwamba wanavunja sheria kwani Serikali kupitia EWURA wamezuia uuzaji wa mafuta ya petroli kwenye chupa za maji, hili linahatarisha maisha ya watu na mali zao,” alisema mmoja wa wateja aliyekuwa anasubiri huduma kwenye kituo hicho.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa Wilaya ya Bariadi waliiomba Serikali kuwabana wafanyabiashara hao, kwani mtindo huo umeshamiri kwenye Wilaya yao, jambo ambalo ni hatari.

“Tupo hatarini sana, petroli inauzwa kiholela kama maji tu na wanaofanya hivi hawana wasiwasi kwasababu huenda kuna watu wanawalinda, tunaiomba Serikali itupie jicho suala hili na itusaidie, maana tunasikia matukio ya watu nyumba zao kuchomwa moto,”

“Wengine wamechoma moto wepenzi wao, sasa kama upatikanaji wa mafuta ni rahisi namna hii, tutarajie matukio mengi zaidi kama hatua hazitachukuliwa,” alisema mkazi wa Bariadi, aliyejitambulisha kwa jina moja la Mabula.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *