MFANYABIASHARA wa madini Deogratias Kulwa Ncheye, mkazi wa Wilaya ya Kahama, Mkoani Shinyanga anadaiwa kumtapeli sehemu ya mgao wa fedha za mauzo ya madini mmiliki mwenza wa leseni ya uchimbaji Abdul Hussein Abdallah, mkazi wa jijini Dar es Saalam.

Madini hayo ni yale ambayo yaliripotiwa Septemba mwaka jana 2024 yaliyopatikana Wilayani Chunya, Mkoani Mbeya ambapo mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu Aidan Andrea Msigwa, alitajwa kuuza Kilo 111.82 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 20.11 katika Soko la madini Chunya.

Kupitia mauzo hayo, Serikali ilipata Shilingi Bilioni 1.2 ikiwa ni mrabaha, Shilingi Milioni 201 ada ya ukaguzi na Shilingi Milioni 60.34 ikiwa ni malipo ya ushuru wa huduma kwa Halmashauri, ambapo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilipata Milioni 402.31 kama malipo ya kodi ya zuio.

Kutokana na mauzo hayo, ambayo yalichimbwa kwenye mpaka wa leseni namba PML2260MBY anayomiliki Msigwa na PML1806 MBY inayomilikiwa na Deogratias Kulwa Ncheye, kwa kushirikiana na Abdul Abdallah, leseni zote zilipata mgao sawa wa Shilingi 9,200,334.00.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo mwandishi wa habari hizi amepata nakala zake, Ncheye ambaye anamiliki asilimia 30 ya hisa za kampuni ambayo wanamiliki kwa ubia alipokea kiasi hicho cha fedha, na kisha alimpatia Abdul ambaye anamiliki hisa asilimia 70, Shilingi Milioni 100.

Mara baada ya kupokea kiasi hicho kilichotumwa kupitia kwenye akaunti yake, Abdul alihoji sababu za kutumiwa kiwango hicho, wakati alitarajia kupata kiwango kikubwa zaidi au nusu ya mgao kulingana na hisa zake, lakini hakupata majibu mazuri kutoka mbia mwenzake.

Inaelezwa, Ncheye moja ya madai ambayo anayatoa ni kwamba, madini hayo hayakupatikana kwenye eneo lao, hivyo Abdul hakustahili kupata mgao, lakini uchunguzi unaonyesha kuwa, leseni iliyotumika kwenye uchimbaji ni ile inayomilikiwa na wawili hao, hivyo alistahili kupata haki yake.

Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa, baada ya wabia hao kushindwana, walifikisha suala lao kwa Afisa Madini Mkazi, Tume ya Madini Mbeya, ambapo Ncheye alitakiwa kumlipa Abdul, lakini hakutekeleza makubaliano hayo.

Jitihada za Abdul kutafuta haki yake ziliendelea ambapo suala lao lilifika kwa Waziri wa Madini ambaye alimuagiza Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini kuitisha kikao cha usuluhishi huko nako Ncheye alionekana ana makos ana kutakiwa kumlipa mbia mwenzake haki yake.

Kwa mujibu wa barua yenye Kumb. Na. HA 242/341/0296 iliyosainiwa na Katibu Mtendaji Ramadhani Lwamo ya Mei 12, 2025, Abdul kupitia kwa wakili wake aliwasilisha hati ya madai ya Shilingi Bilioni 13.2.

Barua hiyo ilielezea makubaliano ambayo yalifikiwa kupitia kikao kilichofanyika Mei 9, 2025 na kuhudhuriwa na Deogratias Kulwa Ncheye, Abdul Hussein Abdallah, Aidan Andrea Msigwa na Heri Hamad Lema ambaye ni Katibu wa Chama cha wachimbaji Madini Mkoa wa Mbeya (MBEREMA).

Kupitia kikao hicho, ikabainika kwamba, Msigwa hahusiki katika mgogoro huo kwa kuwa kila leseni ilipata mgao sawa wa fedha zilizopatikana katika uzalishaji wa madini na Ncheye alikiri kupokea malipo stahiki yaliyohusisha leseni namba PML 1806 MBY.

“Mgogoro unawahusu Bw. Deogratias Kulwa Ncheye na mmiliki mwenza wa leseni Abdul Hussein Abdallah kwa kuwa Bw. Ncheye ana makosa ya kutotoa mgao sawa uliotokana na uzalishaji uliofanyika katika maeneo ya leseni PML 1806 MBY, Bw. Abdul alikuwa tayari mgogoro usuluhishwe katika kikao hicho, hata hivyo mmiliki mwenzake wa leseni hakuwa tayari,” ilisema barua hiyo.

Baada ya kusikiliza pande zote za mgogoro, kikao hicho kilikubaliana, Msigwa aendelee na shughuli zake za uchimbaji ndani ya leseni yake PML 2260 MBY kwa mujibu wa sheria ya Madini, Sura ya 123 na Kanuni zake bila kubughudhiwa.

“Bw. Deogratias Kulwa Ncheye amlipe mmiliki mwenzake wa leseni Bw. Abdul Hussein Abdallah mgao wake kutoka kwenye fedha kiasi cha Shilingi 9,200,334.00 alizopokea kutokana na uzalishaji kwa mujibu wa makubaliano yao katika leseni wanayomiliki,” ilisomeka barua huyo na kusisitiza “kwa barua hii, mnashauriwa kuzingatia makubaliano yaliyoainishwa.”

Hata hivyo, pamoja na jitihada hizo za Abdul na Serikali kuhakikisha kila upande unapata haki yake, bado Ncheye anaonekana wazi hayupo tayari kumlipa mmiliki mwenza haki yake, jambo ambalo limetafsiriwa kuwa ni utapeli ambao inadaiwa amekuwa akiufanya kwa watu mbalimbali.

Mwandishi wa habari hizi alipomtafuta Deogratias Kulwa Ncheye kupitia simu yake ya mkononi hakufanikiwa kumpata, ambapo jitihada zinaendelea ili kujibu kuhusu suala hilo la kutotekeleza makubaliano ya kikao kilichoitishwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini na tuhuma nyingine nzito za mfanyabiashara huyo ambazo tunaendelea kuzifuatilia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *