TIMU ya mpira wa kikapu Wasichana kutoka Mkoa wa Arusha, imetetea ubingwa wake baada ya kuifunga Mwanza katika mchezo wa fainali ya mchezo huo iliyofanyika Juni 17, 2025.
Mchezo huo wa Fainali umechezwa katika uwanja wa Sekondari Lugalo-Iringa, ambapo Arusha ilishinda kwa vikapu 55 kwa 17 katika mchezo uliokuwa wa kusisimua.
Arusha wamefanikiwa kushinda kombe hilo kwa mara ya pili mfululuzo, baada ya kufanya hivyo katika mashindano ya mwaka uliopita yaliyofanyika Mkoani Tabora.
Kocha wa timu ya Mkoa wa Arusha Lekumock Laizer, ameelezea ushindi huo kuwa ni matokeo ya kujiandaa na kujituma ambako kumekuwa kuifanywa na timu yake chini ya viongozi wa mkoa.
Kwa upande wake Kocha wa timu ya Mwanza Ndugela Mndobesya ameipongeza Arusha kwa ushindi huo, akisema kuwa waistahili kutokana na kuwa na kikosi kilichokamilika.
“Nawapongeza Arusha, walistahili ushindi huu kutokana na ukubwa wa kikosi chao ambacho kinawapa urahisi wa kufanya uchaguzi na mzunguko wa wachezaji jambo ambalo ni faida kubwa kwao”