KATIKA mwendelezo wa dhamira yake ya kuendeleza vipaji na kukuza utafiti nchini, kampuni ya Barrick nchini imekuwa mmoja wa wadhamini wa maadhimisho ya kumi ya wiki ya Utafiti na Uvumbuzi.

Maadhimisho hayo yameandaliwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo Barrick imetunukiwa cheti cha tuzo kutokana na udhamini huo.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, Barrick imetoa Shilingi Milioni 10 kwa mmoja wa washindi katika utafiti ambaye ni Dkt. Juma Mmongoyo, kutoka Mkwawa University College of education (MUCE) kwa mradi wake wa utafiti kuhusu “Mbinu za kudhibiti mdudu mharibifu wa nyanya kwa ajili ya ukuaji wa zao la nyanya mkoani Iringa.”

Barrick mbali na udhamini huo imekuwa ikidhamini programu mbalimbali za utafiti , uvumbuzi na inazo programu za mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu na vya kati kwenye migodi yake nchini ya North Mara na Bulyanhulu.

Migodi hiyo inaiendesha kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals, pia imekuwa kila mwaka ikifadhili semina za kuwajengea wanafunzi wa vyuo vikuu uwezo kupitia taasisi ya AIESEC Tanzania.

Semina za AIESEC zinazoendelea katika vyuo vikuu mbalimbali nchini zinazidi kuwapatia Wanafunzi utambuzi wa kujua fursa zilizopo nchini na jinsi ya kuzitumia kuendeleza maisha yao, kupata ajira, kujiajiiri na kutengeneza fursa za ajira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *