Na Mwandishi Wetu

WANACHAMA wanne wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Nanyumbu, Mkoani Mtwara, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kutoa taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii.

Wanaoshikiliwa ni Mustapha Nyalila ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi Wilaya ya Nanyumbu, Hamza Nyalila Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya na Fatma Kaindi.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo tumezipata sambamba na ushahidi wa baadhi ya majibizano ya wanachama hao kupitia kwenye kundi la mtandao wa kijamii wa whatsapp linaloitwa ‘OFISI YA MBUNGE NANYUMBU’, watuhumiwa hao wanadaiwa kumkashifu Mjumbe wa Halmashauri Kuu Wilaya ya Nanyumbu Salvador Lyimo.

Kupitia kwenye kundi hilo, wanachama hao wanadaiwa kutoa tuhuma (ambazo hatuwezi kuziweka hadharani kwasababu za kimaadili) zenye lengo la kumdhalilisha na kumvunjia heshima Lyimo kwa jamii ya jimbo hilo, huku ikidaiwa chanzo ni sababu za kisiasa.

“Pale kinachoendelea ni masuala ya kisiasa tu, wanataka kumchafua mwenzao ili kama itatokea kwenye uchaguzi ujao anataka kugombea nafasi yoyote ya uongozi, akose sifa,” alisema mmoja wa wanachama wa CCM, Nanyumbu ambaye aliomba hifadhi ya jina lake.

Alisema, mbali na tuhuma hizo dhidi ya Lyimo, kwa muda mrefu kikundi hicho cha watu ambao wanatajwa kuwa ni wapambe wa Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Yahya Mhata, wamekuwa wakimbagua Lyimo kwasababu anatoka Kanda ya Kaskazini.

Mwanachama huyo alisema, wamekuwa wakimtolea maneno ya kibaguzi na kumtaka akagombee kwao kwa maana ya Mkoa wa Kilimanjaro, jambo ambalo limekuwa likimuhuzunisha, kwani vitendo hivyo ni kinyume na Katiba ya nchi ambayo inamruhusu Mtanzania yeyote kwenda kuishi popote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kugombea nafasi yoyote ambayo ataona inaendana na sifa alizonazo.

“Pia, wanachofanya ni kinyume na ahadi ya CCM ambayo inasema binadamu wote ni sawa, sasa kwanini wanambagua mwanachama mwenzao kisa tu ametoka mkoa mwingine?” alihoji mwanachama huyo.

Mwandishi wa habari hizi alipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara Issa Suleiman, alithibithisha kutokea kwa tukio hilo ambalo jalada lake limefunguliwa kwenye kituo cha polisi Mangaka kwa namba MKA/09/2025 na MKA/IR/08/2025, ingawa hakuwa tayari kutoa taarifa zaidi kwa madai kwamba, suala hilo ni dogo na linashughulikiwa, hivyo halipaswi kuripotiwa kwenye vyombo vya habari.

Kwa upande wake Mbunge wa Nanyumbu Yahya Mhata alipotafutwa kwa simu yake ya mkononi ili kuthibitisha kama anawatambua watu hao na kundi husika, simu yake iliita bila majibu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *