Ujenzi wa jengo la ghorofa mbili ukiendelea huku chini ya jengo hilo kukiendelea shughuli za Supermarket bila kuwepo tahadhari zozote.
Wakati taifa likiwa bado lina majonzi ya kupoteza watu waliofariki kwenye jengo lililoporomoka Kariakoo, bado ujenzi holela unaendelea kufanywa jijini Dar es Salaam.
Morningstar Post, imeshuhudia ujenzi wa ghorofa mbili, mtaa wa Ursino Estate Kinondoni, Jijini Dar es Salaam, unajengwa huku kukiwa hakuna tahadhara zozote za usalama wa watu,
Mafundi walioko kwenye ujenzi huo walionekana kutokuwa na vitendea kazi, kama buti, kofia ngumu, na nguo za kazi hali ambayo ni hatarishi kwa maisha yao.
Aidha, wakati ujenzi huo ukiendelea huku kukiwa na shughuli za ‘Supermarket’, eneo la mradi huo hakukuwa na bango linaloonesha kuwa kampuni gani ya ujenzi inayosimamia ujenzi huo.
Hata hivyo katika hali ya kushangaza wakati ujenzi ukiendelea, shughuli za supermarket nazo zinaendelea huku mwandishi wa habari hizi alishuhudia mbwa wakiranda randa ndani ya supermarket hiyo ambayo vinauzwa vitu mbalimbali.
“Mimi hata vitu vya humo ndani siwezi kununua, mbwa muda wote wanazunguka humo na kunusa vitu kwa sisi waislamu hatuwezi kununua” alisikika mtu mmoja kwenye eneo la supermarket hiyo ambaye alikataa kutaja jina lake.
Akizungumza na Morningstar Post, Msimamizi wa Supermarket hiyo, ambaye ni raia wa Chini, alijtambuisha kwa jina moja la Tonny, alikataa kuzungumza lolota akamtaka mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na injinia anayesimamia ujenzi wa jengo hilo.
Akizungumza na Morningstar Post kwa njia ya simu, Injinia Flowin Tibinura, alisema kibali cha ujenzi wa jengo hilo kipo na wakaguzi kutoka Manispaa ya Kinondoni huwa wanafika kukagua mara kwa mara.
Hata hivyo, alishindwa kutoa maelezo zaidi kuhusu kutokuwepo kwa alama za tahadhari, uzio wa usalama na wafanyakazi kutokuwa na vitendea kazi.
Mornginstara Post inaendelea kufuatilia mamlaka zinazohusika kuhusu ujenzi huo.