Na Mwandishi Wetu
“Huoni kwamba Mhe. Waziri wakati umefika wilaya ya Nanyumbu ikaanzisha chama chake cha ushirika ili kuwa karibu zaidi na wananchi”
Hii ni kauli ya mbunge wa Nanyumbu Mhe. Yahya Ali Mhata alipokuwa akiuliza swali la nyongeza kwenye kikao cha bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hivi karibuni.
Mhe. Mhata alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuboresha maendeleo ya zao la korosho na kwa kuwa bei ya korosho inachangia maendeleo ya wakulima wa zao hilo serikali ina mpango gani wa kupanga bei elekezi.
Katika swali la nyongeza Mhe. Mhata alitaka kujua serikali inazungumzia nini suala la wakulima wa korosho wilaya ya Nanyumbu kujitenga na Chama Kikuu cha Ushirika (MAMCU), na kuanzisha Chama chao wilaya Nanyumbu ili kuwa karibu zaidi na wananchi.
Mhe. Mhata alitoa hoja hiyo akiangalia kigezo cha chama kuwa karibu zaidi na wananchi, lakini alisahau kuwa kwa wakulima wa Nanyumbu kujitenga na MAMCU kutadhoofisha maendeleo ya Chama hicho ambacho kwa hivi karibu kimejimarisha sana kiuchumi.
MAMCU hivi karibuni waliweza kujiimarisha sana kiuchumi kwa kuwa na shamba la kimkakati la hekari 500 wamefanikiwa kupanda ufuta hekari 200 na mbaazi hekari 300 ambazo zimepandwa kwa kufuata utaratibu na mategemeo mpaka 2025 watakuwa wamelima hekari 700.
Vyama vikimiliki mashamba makubwa kama la MAMCU itasaidia kupunguza makato kutoka kwa wanachama ila pia itarahisisha upatikanaji wa mbegu hali itakayopelekea kumpunguzia mwanachama gharama za uzalishaji wakati wa kupanda.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa kauli hiyo ya mbunge ya Nanyumbu Mhe. Mhata ina mlengo wa kisiasa na sio kuwasaidia wananchi wa Nanyumbu.
Wanasema viongozi walioshindwa kuleta maendeleo MAMCU wanataka kurudi kuongoza kwa mlango wa nyuma hivyo wanashinikiza kuanzishwa kwa chama kipya ili washike tena madaraka ya kuongoza kwa maslahi yao binafsi.
Hata hivyo, uanzishwaji wa chama kipya utategemea na maoni na kuwashirikisha wakulima wa Nanyumbu,
Serikali inapaswa kuchunguza kwa kina kauli hii ya Mhe Mbunge licha ya kutokuwa na pingamizi la kuanzishwa kwa chama kipya cha ushirika Nanyumbu.
Aidha, uongozi wa Morningstar Post, unajipanga kutuma timu ya waandishi wa habari mkoa wa Mtwara kuzungumza na viongozi wa MAMCU na kuchunguza kwa nini Nanyumbu wanataka kujitenga kuanzisha chama kipya.