
Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Halima Okash amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze Ndugu Ramadhani Poss kumuandaa Mwanasheria na kuzipitia upya Nyaraka walizonazo ( CHAURU) ili kujiridhisha zaidi katika kutatua mgogoro uliopo baina yao na wananchi wa kata ya vigwaza.
Ameyasema hayo leo Julai 18,2024 alipotembelea maeneo ya vitongoji vya Kwazoka, Visezi Kiloweko,Ruvu darajani na kitongoji cha Kilimani Vya kata ya Vigwaza na kusikiliza kero zao huku wengi wao wakituhumu Chama Cha Ushirika (CHAURU) kuwa kinamiliki Ardhi kubwa hivyo kusababisha baadhi ya huduma za kijamii kushindwa kutekelezeka kutokana na ukubwa wa eneo hilo ambalo si mali ya kijiji.
Aidha Mhe Okash amewashauri na kuwasihi wananchi hao kuwa watulivu ili kutatua mgogoro uliopo baina yao na Chama Cha Ushirika (CHAURU) ambacho kina Hati na umiliki halali kwa mujibu wa Sheria.
Kadhalika Mh Halima Okash ameitaka mamlaka ya Barabara vijijini (TARURA) waangalie namna gani ya kuweka Daraja ambalo Wananchi wameorodhesha kama kero kwao kwani Watoto wanapata shida ya kuvuka pindi Mvua zinaponyesha kwa wingi na kusababisha wanafunzi kutofika shuleni kwa wakati.
Pia amewataka DAWASA NA RUWASA kufuatilia kero ya Maji kwa ukaribu Zaidi kwa kuongea na Wananchi ni lini Maji yataanza kupatikana na ameahidi kurudi ili kufuatilia utekelezaji wa maelekezo yake.