Na Mohammed Ussi, MeCAP

BAADHI ya wananchi jijini Dar es Salaam wameziomba mamlaka husika kuliweka jiji hilo katika hali nzuri zaidi kwa kuziondoa karakana za kutengeneza magari zilizozagaa mitaani katika Jiji hilo.

Wakiongea na Morning Stars, wananchi hao wamesema Hali ya Jiji la Dar es Salaam inazidi kuwa chafu kutokana na Halmashauri za Jiji hilo kubwa kibiashara hapa nchini kuwaachia wafanyabiashara wakiwemo wamiliki wa gereji hizo kuendelea kufanya shughuli zao kiholela.

“Hali ni mbaya zaidi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ambako mitaa mingi ya wilaya hiyo imegeuzwa kuwa gereji. Lakini hata Ilala pia na Kinondoni kidogo”, amesema mdau wa Mazingira, Dk. Alan Chala.

Amesema hajui ni vigezo gani vinatumika kuwapa ridhaa wafanyabiashara hao kufanya shughuli zao kwenye makazi ya watu, ingawa amesema inaweza kuwa ni woga wa serikali za mitaa kuchukua hatua.

“Wakati mwingine ni woga tu kwamba hawa wafanyabiashara ndiyo wananchi wenyewe, ndiyo wapiga kura wenyewe, lakini pamoja na hayo lazima wawekewe utaratibu mzuri kwa ustawi wa Jiji Zima” , amesema.

Meneja Miradi wa Kituo cha Habari dhidi ya Umasikini (MeCAP), David Mbiza amesema Shirika lake limeandika pendekezo la namna ya kuboresha mazingira na usafi katika majiji yote makubwa, na pendekezo hilo litawasilishwa kwenye mamlaka husika hivi karibuni.

“Tumefanya utafiti na tumeandika wazo la jinsi gani majjiji haya na halmashauri nyingine zinaweza kuwa katika Hali Bora kabisa. Tutawasilisha mapendekezo hayo kwa serikali” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *