
Baadhi ya washiriki wa semina ya ushirikiano kati ya China na Tanzania katika elimu ya ufundi iliyofanyika jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo Stadi, Bernadeta Ndunguru
Na Mdoe Kiligo, MeCAP
MOJA ya mambo yanayotajwa kwamba yamekuwa chachu ya maendeleo ya taifa lolote ni pamoja na jinsi ambavyo wananchi wa taifa hilo wanathamini lugha na utamaduni wao.
Utamaduni ukitumika vizuri kuanzia kwenye makuzi ya watoto hadi wanakuwa vijana, na utamaduni huo ukisanifiwa na lugha inayomfanywa mtoto kufahamu kile anachokifanya, faida yake ni kwamba mtoto huyo atatumia kipaji chake kwa ustawi wake yeye mwenyewe na taifa lake kwa ujumla.
Wiki iliyopita nilibahatika kuhudhuria kwenye semina ya siku moja iliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo Stadi (NACTVET) kwa ushirikiano na Wadau wengine wa Sekta ya Elimu ya Ufundi kutoka nchini China.
Katika semina hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, zaidi ya vyuo 10 vya elimu ya ufundi kutoka nchini China, pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo wafadhili wa Elimu nchini humo na hapa nchini, walihudhuria.
Akifungua semina hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe akasema kwamba ushirikiano wa Tanzania na China katika sekta ya ufundi umeinufaisha zaidi Tanzania.
Profesa Mdoe ambaye alimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda aliisifu China kwa kutumia wataalam wake kuisaidia Tanzania katika miradi mbalimbali ya Elimu ya Ufundi kwa nia ya kukuza kiwango cha elimu hapa nchini, lakini pia kuleta maendeleo kwa ujumla.
Akasema ujio wa wadau hao wa elimu ya za ufundi kutoka China utasaidia sana kuifanya Tanzania kupata maendeleo ya kiufundi na kiteknolojia na akalisifu Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo Stadi kwa ubunifu na umahiri kwenye kuendeleza elimu ya ufundi, ubunifu na ujuzi hapa nchini.
Naye Mwenyetiki wa Baraza hilo la Elimu ya Ufundi hapa nchini Bernadeta Ndunguru amesema ushirikiano huo mkubwa baina ya China na Tanzania unaibeba zaidi nchi yetu akiamini kwamba Watanzania tuna kitu cha kujifunza kutoka nchini China kupitia wadau wa elimu ya ufundi kutoka nchini humo, lakini akaisifu menejimenti na sekretarieti nzima ya NACTVET kwa kufanikisha semina hiyo.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa NACTVET Dk. Adolf Rutayuga amesema hiyo ni mara ya pili kwa semina hiyo kufanyika hapa nchini, na kupitia kwayo Watanzania na Wachina wameweza kubadilishana uzoefu na ujuzi ambao umevisaidia sana vyuo vya elimu ya ufundi hapa nchini.
“Wawakilishi wa vyuo zaidi ya kumi kutoka nchini wako hapa, ni fursa kwa wadau wa hapa nchini kukutana nao na kubadilishana ujuzi na uzoefu kwa manufaa ya pande zote mbili” Dk Rutayuga amesema.
Mmoja wa wakilishi kutoka nchini China, Bw. Xiaoping Man ambaye ni Mkuu wa Idara ya Lugha za Kigeni katika Chuo cha Jining Polytechnic amemwambia mwandishi wa Makala haya kwamba anatamani kuona Tanzania inakuwa bora zaidi katika sekta ya elimu ya ufundi, lakini akasema China imefanikiwa zaidi kwa kutumia lugha na utamaduni wake.
“Sisi Wachina tumefanikiwa katika mambo mengi kwasababu hata bidhaa zetu zinazouzwa ndani ya soko, zimeandikwa kwa Kichina, lakini hata zinazokwenda nje ya nchi zinasomeka kwa Kichina na ufafanuzi wa labda Kiingereza na lugha nyingine” amesema na kuongeza:
“Kwa nyie Tanzania, bado mnaweza kutumia lugha yenu ya Kiswahili inayozungumzwa na wananchi wengi zaidi katika kukuza soko la ndani la bidhaa zenu, na mnaweza kutumia lugha za kigeni katika kuuza tu bidhaa nje za nchi yenu”.
Kauli hii ya Bw. Xiaoping inatufungua macho watanzania kwamba wakati umefika sasa tunapozalisha bidhaa zetu viwandani kutokana na elimu bora ya ufundi ambazo tumeipata tusisahau kwamba tuna mtaji mkubwa ambao ni Kiswahili.
Kwamba ni kweli kabisa wenzetu China wamefanikiwa sana kukuza soko la bidhaa zao ndani na nje ya China kwasababu ya mtaji wa lugha yao, vivyo hivyo kwa nchi nyinginezo.
Chukulia mfano mdogo, hapa kwetu kiwanda kinachozalisha bidhaa ambayo mlaji wake ni Mtanzania wa kawaida, mswahili kabisa inatengenezwa kwa maelekezo ya lugha ya kiingereza ambazo mlaji wa kawaida haifahamu.
Maji ya kunywa, juisi, unga wa sembe au hata kiberiti bidhaa ambazo zinaishia kuuzwa ndani ya mipaka yetu zinafungashwa katika makasha ambayo yameandikwa kwa Kiingereza, lugha ambayo ni ngumu kwa mlaji wa kawaida sana.
Kama tunataka kuisaidia nchi yetu, ni ukweli kwamba tuna kitu cha kujifunza kutoka kwa wenzetu ambao wameendelea zaidi yetu wakiwemo Wachina.
Kiswahili bado ni mtaji mkubwa kwa maendeleo yetu, na mtaji huu unatakiwa kuanza kujengewa mazingira mazuri kuanzia katika shule za awali mpaka vyuo vikuu, kwamba pamoja na kutumia lugha nyingine za kigeni kama sehemu ya kujifunzia mambo mbalimbali, lakini inawezekana kuwawa na kozi ambazo wanafunzi wakifundishwa kwa Kiswahili wanaweza kuwa waelewa zaidi, lakini pia kama alivyosema Dkt Rutayuga vyuo vya ufundi hapa nchini vina jambo la kujifunza kutoka kwa wenzetu hao.
Ujuzi unaotajwa kwenye mafunzo haya ni zile mbinu ambazo wataalam wanawafundisha wanafunzi mbalimbali, lakini wenyewe wahitimu wanapofika kwenye ajira wanatakiwa kuwa wabunifu zaidi ili kuongeza tija, na ubunifu ni pamoja na kutumia kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia hata kwa kuwasiliana na marafiki wengine wa nchi katika kubadilishaba uzoefu na ujuzi.