Na Mdoe Kiligo

WAZIRI Mkuu Kasim Majaliwa amewataka Watendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo Stadi (NACTVET) wahakikishe kuwa washindi wa Mashindano ya Ujuzi watakaopata fursa ya kushiriki Kikanda na Kimataifa wanaandaliwa vizuri ili wakaiwakilishe vyema nchi yetu na kurudi na ushindi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo katika kilele cha wiki ya Elimu na Ujuzi iliyofanyika Jijini Tanga, maonesho ambayo yamepongezwa na wadau wengi kwamba yamefanikiwa kwa kiwango kikubwa.
Maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yalianza tarehe 25 Mei na kufungwa tarehe 31 Mei 2024, yakiwa yamefanyika kwa mara ya kwanza mkoani Tanga, yakihusisha wadau wote wa Elimu nchini vikiwemo Vyuo Vikuu, Vyuo vya Kati, Taasisi na Mashirika ya Elimu.
Akizungumza wakati alipotembelea Banda la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Mhe. Majaliwa amekipongeza Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kuweza kubuni vifungashio mbadala ambavyo ni rafiki kwa Mazingira, na hivyo kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Aidha, ametoa wito kwa UDOM kuendelea kufanya tafiti na kuja na bunifu nyingi za kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii, likiwemo suala la vijana kujiajiri.
Naye, mbunifu wa vifungashio hivyo kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma ambaye ni Mkufunzi Msaidizi Bw. Mohammed Amini, kutoka Ndaki ya Sayansi Asilia na Hisabati amesema vifungashio hivyo vinatengenezwa kwa malighafi taka na zao la mwani na hivyo gharama za kuzalisha ni ndogo kiasi cha kila mwananchi kuzimudu, na pia ni bidhaa rafiki katika kutunza mazingira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *