Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Adolf Rutayuga

Na Mdoe Kiligo, MeCAP.

TANGU mwaka 1964 wakati Tanganyika na Zanzibar zilipoungana na kuzaliwa Tanzania hadi leo, Muungano umesaidia sana kuwaweka Watanzania kuwa kitu kimoja.

Watanzania wameungana katika mambo mengi ya msingi, na kipitia Muungano huu wamekataa na kuyashinda mambo mbalimbali magumu.

Ndiyo, zipo nyakati ngumu ambazo taifa letu limepita, na tumefanikiwa kuvuka nyakati hizo ngumu kirahisi kwasababu Watanzania wamekuwa wamoja, na wameshikamana vya kutosha kutokana na Muungano wetu.

Huduma nyingi za kijamii kama Elimu, Afya, Fedha na Mawasiliano, lakini pia shughuli za ulinzi na usalama wa nchi yetu vimepewa kipaumbele zaidi katika nyakati zote za uhai wa Muungano wetu, na Watanzania wamehudumiwa kupitia sekta hizo na nyingine bila kubaguliwa.

Hata zile kero za Muungano ambazo tumeishi nazo baada ya kuasisiwa kwa Muungano wenyewe ni kama zimepungua sana ama hazipo, tena na kama zipo basi hazina madhara kwa maisha na maslahi ya Watanzania wenyewe.

Katika miaka hii 60 ya uhai wa Tanzania, kuna mambo mengi yamefanyika. Tulivyokuwa mwaka 1964, sivyo tulivyo leo hii.

Hakuna asiyejua kwamba ili kuimarisha taifa hili kiuchumi, serikali ililazimika kupambana na kuzalisha wasomi wengi zaidi ambao wamekuja kushika nafasi mbalimbali kuanzia mashambani, ofisini na viwandani.

Ikumbukwe kwamba wakati tunaungana mwaka 1964, nchi hii haikuwa na wasomi wengi, na hata wale waliopewa dhamana ya kushika nafasi mbalimbali za kisiasa na kiutendaji wakati ule walikuwa na elimu ya kawaida sana.

Viwanda ambavyo tulijenga viliongozwa na wataalam wengi kutoka nje na tukawapa jina la “Ma-TX”, ambao walikuwa wakisaidia kuwapa ujunzi wa nadharia watanzania wachache waliokuwa wanafanya nao kazi.

Ili kuondoa utumwa huo, serikali ikaweka mkazo kwenye kuongeza vyuo vya ufundi na kuimarisha vile vilivyokuwapo, lakini mabadiliko mbalimbali ya sheria yalisaidia pia kuanzishwa kwa taasisi ambazo zilisimamia elimu ya ufundi ili kuiwezesha Tanzania kuwa na wasomi wengi kwa ajili ya kukamata soko la ajira na kusimamia uchumi wa nchi.

Kwa mfano, serikali ilianzisha Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ambalo sasa linaitwa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo Stadi (NACTVET), kwa nia ya kuratibu na kusimamia elimu ya ufundi hapa nchini.

Meneja Mawasiliano wa Baraza hilo Jeff Shelembi amesema NACTVET imesaidia sana kuongeza soko la ajira hapa nchini, lakini usimamizi na uratibu wake umesaidia kuwafanya Watanzania sasa kuwa wamiliki wa viwanda ama kuajiriwa kwenye viwanda mbalimbali wakitoa ujuzi na ufundi wao, badala ya taifa kuwategemea wageni kufanya kazi kwenye viwanda vyetu.

Hata katika sekta ambazo sio za viwanda kwa maana ya huduma za jamii na maeneo mengine, wasomi wengi wameajiriwa huko Tanzania Bara na Visiwani na wamekuwa wakitoa huduma kwa weledi mkubwa, kutokana na elimu bora ya ufundi ambayo wameipata katika vyuo vyetu.

NACTVET ambalo Katibu Mtendaji wake ni Dkt Adolf Rutayuga ni Baraza ambalo utendaji wake umeibeba sana nchi hii.
Wakati tunasema nchi yetu inakwenda kuwa nchi ya uchumi wa kati ukibebwa na viwanda, lazima tukubali kwamba viwanda hivi lazima viendeshwe na wasomi ambao wamepata ujuzi katika viwanda vyetu.

Taasisi zinazotoa huduma pia zimeajiri wasomi wenye weledi wa kutosha kwasababu wasomi hao wametoka kwenye vyuo vilivyosimamiwa na kuratibiwa vema na Baraza hilo.

Leo hii Watanzania wanatoka Tanzania Bara na kwenda Zanzibar kufanya kazi kwenye sekta mbalimbali, kama ambavyo Wazanzibari wanakwenda upande wa pili wa Muungano kufanya kazi kutokana na ujuzi ambao wameupata katika vyuo mbalimbali vilivyotapakaa Tanzania Bara na Visiwani.

Hata Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Wizara hiyo itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Mageuzi ya Elimu yanayoenga kupata wahitimu wenye ujuzi na mahiri katika nyanja mbalimbali.

Mkenda amesema hayo Aprili 05, mwaka huu jijini Dodoma akifunga Mkutano wa mwaka wa pamoja na wadau wa Tathimini ya Sekta ya Elimu kwa mwaka 2023/24, ambapo amesema serikali itaendelea kushirikiana na Wadau kuhakikisha inatoa Elimu bora, ikiwemo Elimu ya Amali inayopewa msukumo sasa ili kuwezesha ujuzi kwa Vijana wa Kitanzania.

Kwahiyo, tunapozungumzia manufaa ya muungano ni pamoja na kuwaunganisha Watanzania zaidi, kuwapa nafasi ya kufanya kazi mahali popote, lakini kusimamia uchumi wa nchi yao wao wenyewe kwa asilimia kubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *