
Na Waandishi Wetu
KWA wiki kadhaa kumekuwa na taarifa zinazotisha kwenye vyombo vya habari kuhusu kile kinachotajwa kuwa ni madhara ya vinywaji vya kuongeza nguvu mwilini “ernegy drinks”.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, kinywaji hicho kinaelezwa kuwa na madhara hasi mwilini hasa katika Figo na Moyo na pia inaelezwa hufanya Damu kuwa nzito mno.
Taarifa hiyo ambayo imechapishwa kwenye baadhi ya magazeti inasema imeshauriwa kiafya kwamba mtu asizidishe chupa mbili kwa wiki na kama hatoweza kuvumilia basi asizidishe kopo moja lenye ujazo wa Mls 250 kwa muda wa saa 24, huku ikishauriwa kwamba chaguo sahihi ni kuepukana na kinywaji hicho kabisa.
Mtaalam wa Afya mmoja aliyezungumza na tovuti hii anasema kinywaji hicho ni hatari ingawa imekuwa mazoea kwamba ndiyo kinywaji pendwa hasa kwa vijana wengi.
“Pamoja na kwamba vinywaji hivi vimekuwa maarufu hasa kwa vijana
kibaya zaidi ni kwamba watumiaji ni watu wenye rika zote, asilimia kubwa hawajui madhara” amesema Dkt Sebastian Shamba.
Amesema mara nyingi kinywaji hicho hupendwa na watu wanaotumia sana akili na nguvu kwenye kazi zao, lakini hawajapata muda wa kujua madhara yake.
Amesema kinywaji hicho kimetengenezwa kwa Caffeine nyingi, pamoja na kemikali nyingine ambazo zina madhara kwenye kila kiungo cha mwili wa Binadamu.
Amesisitiza kuwa kwa ujumla “ernegy drinks” hazifai kwa matumizi ya kila siku kwa binadamu, kwani kuna vimelea vya URAIBU, hali ambayo inaweza kusababisha mtu kuihitaji wakati wote.
Kauli hiyo imeungana na ile ya Dk Pedro, ambaye pia ni mkuu wa Kitengo cha Utafiti Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), aliyekaririwa na gazeti moja akisema unywaji wa vinywaji vya kuongeza nguvu huathiri mifumo yote kwenye mwili.
Alisema kwenye mwili kinywaji hicho husababisha kufeli ghafla kwa Figo, kukosa Usingizi, kuharisha na kutapika, kichwa kuuma, mfumo wa chakula kuathirika, pia kutokea kwa vifo via ghafla na kuwa na mawe kwenye Figo “Kidney Stones.”
Pia Dk Pedro Palangyo alisema “matukio ni mengi, lakini JKCI walichapisha kisa kimoja ambacho kilimhusisha kijana mwenye umri wa miaka 28 aliyeziba mshipa wa Moyo kutokana na kutumia kiasi kikubwa cha kinywaji hicho kwa kunywa kopo tano ndani ya masaa manne.
Naye Daktari Bingwa wa maswala ya Wanawake, Dk Hanson Mwakifuna alisema kuna madhara kwa Wajawazito kutumia “Energy Drinks” kwa sabbat ya wingi wav Caffeine ambayo ni hatari kwao.
“Huwa tunawashauri wajawazito kutotumia vinywaji au vitu vyenye Caffeine kwa ajili ya kumlinda mtoto kwani inaweza kumsababishia maumivu ya kichwa, mapigo ya moyo kwenda mbio, kujifungua kabla ya wakati, kujifungua mtoto aliyefariki na kujifungua mtoto chini ya Uzito.”
Hoja hapa ni kwamba wazalishaji wa vinywaji hivyo hapa nchini wanajua madhara hayo ya kitaalamu yanayosemwa na madaktari?