Na Mwandishi Wetu
Mwaka 2023 umeondoka, tumeanza mwaka mwingine tena 2024, kwa watanzania tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kuwa tumeendelea kuenzi, urithi wa malezi bora ya waasisi wa taifa hili waliotuachia wa kuikumbatia amani yetu.
Amani na utulivu wetu umeendelea kutuweka salama, licha ya maumivu ya kupanda kwa gharama za maisha.
Watanzania bado tunaheshimu na kudumisha amani ya taifa hili kama silaha ambayo inatulinda katika nchi yetu licha ya kupitia magumu ya maisha kwa watanzania walio wengi.
Wakati huu tunaoanza mwaka 2024 tunapaswa kujiuliza kuwa mwaka uliokwisha tumeweza kutimiza malengo ya kila mmoja wetu, malengo ya ngazi ya familia na malengo ya kitaifa.
Pia, tunapaswa kupanga malengo ya mwaka huu ambayo tunatakiwa kuanza mara moja kuyaendea malengo hayo ya mtu mmoja mmoja na malengo ya kitaifa.
Tukumbuke kuwa huu ndio mwaka ambao unatarajiwa kuwa ndio mwaka wa kujiandaa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais mwakani, ni mwaka ambao unatakiwa kuhakisha tunapanga malengo yetu kwa usawa na uhakika.
Hata hivyo watanzania tunapaswa kutambua kuwa tumeanza mwaka huu 2024 tukiwa katika hali ngumu sana gharama za maisha zimekuwa juu sana na kipato cha mtanzania wa kawaida kinazidi kushuka.
Ajira kwa vijana zimekuwa ni shida, kipato cha mtanzania wa kawaida hakitoshi kukidhi mahitaji kutokana na kupanda kwa bidhaa mara kwa mara.
Tumeshuhudia kupanda kwa nauli za daladala , kupanda kwa bei ya vyakula ambavyo imekuwa ni changamoto kubwa kwa watanzania waliowengi wenye kipato cha hali ya chini.
Tumeshudia mwaka jana bei ya mafuta imepanda nchini Tanzania huku mfumuko wa bei nchini ukikua kwa wastani wa asilimia 3.7 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.3 mwaka 2020, watu kulalamikia sana ongezeko kubwa la gharama ya maisha.
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan alipozungumzia suala hili alisema kuwa wananchi wa taifa hili waambiwe ukweli juu ya kupanda kwa gharama za maisha na bidhaa kote ulimwenguni.
Mafuta yalipanda bei hadi kufika lita moja yaliyopakuliwa Dar es Salaam shilingi 3,281/lita ya petroli, na shilingi 3,448/lita ya Dizeli
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania(EWURA) ilisema kuwa mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi Oktoba 2023 yanatokana na kupanda kwa gharama za mafuta katika soko la dunia kwa hadi kufikia asilimia 4.21 na gharama za uagizaji wa mafuta hadi kufikia asilimia 17 kwa petroli, asilimia 62 kwa dizeli na asilimia 4 kwa mafuta ya taa.
Hivyo tunapaswa kujiuliza na kupanga vizuri mikakati ya kudhibiti hali hii ya mfumo wa bei wa bidhaa na kupanda kwa gharama za maisha kwa watanzania.
Karibu mwaka 2024 uwe ni mwaka wa amani na mafanikio kwa watanzania.