Na MWANDISHI WETU
KLABU ya Mamelodi Sundowns wamefanikiwa kutwaa taji la michuano mipya, Ligi Soka Afrika (African Football League), baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco Uwanja wa Loftus Versfeld jijini Pretoria, Afrika Kusini.
Mabao ya Mamelodi yamefungwa na mshambuliaji wa Kimataifa wa Namibia Peter Shalulile dakika ya 45 na Aubrey Modiba dakika ya 53.
Mamelodi wanakuwa washindi wa kwanza wa African Football League, michuano inayoandaliwa kwa pamoja na FIFA na CAF kwa ushindi wa jumla wa 3-2, kufuatia kufungwa 2-1 kwenye mchezo wa kwanza Jumapili iliyopita jijini Casablanca nchini Morocco.
Kwa ushindi huo, Mamelodi wanapata zawadi ya dola za Kimarekani Milioni 4, wakati Wydad inapata dola Milioni 3.
Timu za Al Ahly ya Misri na Esperance ya Tunisia zilizoishia Nusu Fainali kila moja inapata dola Milioni 1.7, wakati TP Mazembe ya DRC, Enyimba ya Nigeria, Petro Atlético ya Angola na Simba ya Tanzania kila moja imepata dola Milioni 1 kwa kushiriki michuano hiyo ya timu nane
