Na Ibrahim Kadilo na Fred Okoth
Sakata la Kampuni ya Wilmar Tanzania Limited inayotuhumiwa kunyanyasa wafanyakazi wake na kukiuka taratibu za ajira kwa wafanyakazi limeingia katika sura mpya.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bw Edward Mpogolo, zinasema suala hilo limefikishwa kwa Mkuu wa Wilaya Ilala hiyo baada ya kupokea malalamiko ya wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Taarifa zinasema kuwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya iliwaandikia burua ya wito kampuni hiyo inayozalisha mafuta ya kula ya Korie iliyoko barabara ya Nyerere maeneo ya vingunguti jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo baada ya kupokea barua hiyo ya wito kampuni hiyo ambayo zamani ilikuwa inafahamika kwa jina la Murzah Oil iliwasilishwa na mwanasheria wao Bi. Lulu Kissambu kujibu tuhuma hizo.
Licha ya mwanasheria huyo kuzungumza na Morningstar Post kabla ya wito kwa mkuu wa wilaya alitetea kampuni hiyo akikanusha tuhuma hizo kuwa kampuni yao inafuata taratibu zote za ajira kwa wafanyakazi wake.
Alipotakiwa na mkuu wa wilaya kueleza kuhusu barua za kuachishwa kazi wafanyakazi wao, bila kuwapa nafasi ya kuzisoma barua zao na kusaini, mwanasheria huyo alishindwa kueleza na hivyo kutakiwa awasilishe barua hizo mbele ya mkuu wa wilaya.
Akizungumza na Morningstar Post hapo awali Bi Kissambu alikiri kuwa Seif Ismail Makala na Hamisi Hamza Mbogo walikuwa ni wafanyakazi wao wakiwa kama madereva na walikuwa na mikataba ya ajira tangu mwaka 2016 na kampuni hiyo.
Bi Kissambu hakutaka kutoa maelezo ya kina, alisema kwa kufupi kampuni yake ina uhakika kuwa wamefuata taratibu zote za sheria ya ajira katika kuwafukuza kazi wafanyakazi hao.
Akijibu tuhuma za madai hayo kuwa mfanyakazi wao Hamis Mbogo alikuwa hawasilishiwi michango yake ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kipindi cha nyuma akiwa ameajiriwa na kampuni ya Murzah, alisema kuwa kampuni yake inaongoza kwa kuwa kampuni kubwa inayowasilisha michango ya wafanyakazi NSSF.
Licha ya wafanyakazi hao kufukuzwa kazi bila barua ya notisi, barua ya kusitisha mkataba wa ajira, bila kupewa haki ya kusikilizwa na kuona barua ya kufukuzwa kazi, na kushtakiwa polisi kwa kuhusishwa na wizi, Mwanasheria wa kampuni hiyo alisema kuwa huo sio unyanyasaji wa wafanyakazi.
Mkuu wa Idara ya Rasilimali watu (HR), Emmanuel Christopher akizungumzia tuhuma hizo alisema kazi ya kushtaki kwa makosa ya jinai ni ya polisi wao kama kampuni hawapaswi kuulizwa kuhusu suala la wafanyakazi wao kupelekwa polisi kwa tuhuma za wizi.
Wakizungumza na Morningstar POST, wafanyakazi wa kampuni hiyo Seif Makala na Hamisi Mbogo walisema kuwa wamenyanyaswa na kufukuzwa kazi bila kufuata taratibu za ajira.
Walisema kuwa walituhumiwa kuiba trela la gari lenye thamani ya sh35/m na kupelekwa polisi lakini polisi wameshindwa kuendelea na kesi hiyo baada ya kuona kuwa hawahusiki katika wizi huo.
Alisema kuwa mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu Bw Emmanuel na Lyamuya waliwaandikia barua ya kuwafukuza kazi bila kuwapa nafasi ya kuisoma barua hiyo na kuona yaliomo badala yake waliwataka kusaini bila kupata nakala wala kusoma barua hiyo.
Walisema kuwa hatua hiyo ya kutakiwa kusaini barua bila kujua kilichoandikwa walikataa, hivyo mpaka wanashindwa kupata haki zao za michango yao iliyopo NSSF.
Walisema kuwa kitendo cha kuwabambikikizia kesi kilifanywa na watu wa idara ya rasilimali watu kwa chuki binafsi lakini hakuna sababu ya msingi ya kufukuzwa kazi.
Wafanyakazi hao wamemuomba mkuu wa wilaya kufuatilia kwa makini suala hilo kwa kuwa linafanywa na watu wa idara ya rasilimali watu ambao wanachuki binafsi na baadhi ya wafanyakazi.
Taarifa zaidi kuhusu Sakata hili zinaendelea katika machapisho yajayo
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bw Edward Mpogolo.