NA Mwandishi Wetu
KIONGOZI wa Azimio la Umoja One Kenya, Bw Raila Odinga, jana alikwepa ‘mtego’ aliowekewa na Rais William Ruto kuhusu masuala yatakayojadiliwa kwenye mazungumzo mapya ya maridhiano.
Hapo jana, Bw Odinga alisisitiza kuwa lazima suala la kupanda kwa gharama ya maisha lijadiliwe kwenye mazungumzo hayo.
Hii ni kinyume na taarifa ya mrengo wa Kenya Kwanza mnamo Jumamosi, iliyoondoa suala hilo katika orodha ya masuala ya kujadiliwa kwenye mazungumzo hayo yatakayoongozwa na aliyekuwa rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo.
Kwenye taarifa hiyo iliyotolewa na Kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa, Kimani Ichung’wa kwa niaba ya mrengo huo, Kenya Kwanza ilitaja masuala matano makuu iliyodai yamekubaliwa baina yake na Azimio.
Masuala hayo ni: Kujadiliana kuhusu kuteuliwa kwa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), utekelezaji wa sheria ya thuluthi mbili kuhusu jinsia, kujumuishwa katika sheria kwa Hazina ya Maeneobunge (NG-CDF), kubuniwa kwa Afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani na kuingizwa kwenye Katiba kwa Afisi ya Kiongozi wa Mawaziri.
Kama Azimio ingekubali masuala hayo, ingeangukia mtego wa Kenya Kwanza kwamba Raila anashinikiza tu mazungumzo ya kujiunga na serikali kupitia mlango wa nyuma au kubuniwa kwa vyeo vya viongozi.
Ijapokuwa Bw Ichungw’a alidai alitoa taarifa hiyo kwa kumnukuu Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Opiyo Wandayi, Azimio jana iliipuuzilia mbali taarifa hiyo, ikidai masuala yaliyojumuishwa ni ya Kenya Kwanza pekee na hayawakilishi kwa namna yoyote maoni ya mrengo huo.
“Hapo juzi (Jumamosi), Kenya Kwanza ilitoa taarifa kupitia kwa Bw Kimani Ichung’wa, iliyodai kuyajumuisha maoni yetu. Tunapuuzilia mbali taarifa hiyo. Azimio haikuhusika kwa vyovyote vile na taarifa hiyo. Masuala yaliyojumuishwa ni yale ya Kenya Kwanza,” ikasema Azimio kwenye taarifa iliyosomwa na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya.
Azimio ilisisitiza kuwa lazima suala la gharama ya juu ya maisha lijumuishwe kwenye mazungumzo hayo, kwani linawaathiri mamilioni ya Wakenya.
Mrengo huo uliorodhesha masuala yake makuu, kuwa yafuatayo: Kupunguzwa kwa gharama ya maisha, serikali kuhakikisha inajumuisha jamii zote nchini katika uteuzi wa nyadhifa kuu serikalini (bila kujali ikiwa maeneo fulani yaliipigia kura au la), ukaguzi kuhusu matokeo ya kura kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, kuteuliwa kwa makamishna wapya wa IEBC, serikali kuheshimu uhuru wa vyama vya kisiasa na mwisho serikali kusitisha ukiukaji wa haki za binadamu (kutokana na dhuluma zilizofanywa na polisi dhidi ya waandamanaji).
Azimio iliilaumu Kenya Kwanza kwa kuwa kikwazo kikuu cha mazungumzo ya maridhiano, ikisisitiza lazima kila upande uwe huru kujumuisha masuala unayotaka yajadiliwe.
“Sisi tumejitolea kushiriki kwenye mazungumzo. Hata hivyo, lazima Kenya Kwanza ikome kutuwekea masharti kuhusu masuala tutakayowasilisha,” akasema Bw Munya.
Hapo jana, iliibuka kuwa Rais Ruto na Bw Odinga walifanya kikao cha pamoja na aliyekuwa rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo kuweka msingi wa mazungumzo.
Bw Munya alifichua kuwa viongozi hao hawakujadili kuhusu masuala yoyote, bali kikao chao kilikuwa tu “matayarisho ya awali” kabla ya mazungumzo rasmi kuanza.
Pia, alifichua kuwa walijadili wakati ambapo duru hiyo ya pili ya mazungumzo itaanza rasmi.
Katika mazungumzo hayo mapya, kila upande utawakilishwa na wawakilishi watano.
Jopo hilo litajumuisha; wawakilishi wanne kutoka nje ya Bunge (wawili kila upande), Viongozi wa Wengi na Wachache kutoka Bunge na wabunge wanne zaidi (wawili kutoka kila upande).
Varugu zinazoendelea nchini Kenya